PERMISSIONS

Urutubishaji madini ya urani nchini yumkini ukafikia asilimia 60 kulingana mahitaji ya taifa

1 week ago 20

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu haitalegeza kamba katika misimamo yake ya kimantiki kwenye maudhui ya nyuklia na itarutubisha madini ya urani hata kufikia asilimia 60 kulingana na maslahi na mahitaji ya nchi.

Ayatullah Ali Khamenei ameyasema hayo leo alasiri katika kikao kilichohudhuriwa na wajumbe wa Baraza Linalomchagua Kiongozi wa Juu wa Iran. Amesema lugha inayotumiwa na Marekani na nchi tatu za Ulaya kuhusu hatua ya Iran ya kupunguza majukumu yake katika utekelezaji wa makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni ya kibeberu, isiyo ya kiadilifu na isiyo sahihi. Ameongeza kuwa, tangu hapo awali na kwa kipindi kirefu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na mafundisho ya Kiislamu ilitekeleza ahadi na majukumu yake, na upande ambao tangu hapo awali haukutekeleza ahadi na majukumu yake ni nchi hizo nne; kwa msingi huo nchi hizo ndizo zinazopaswa kulaumiwa na kusailiwa. 

Ayatullah Khamenei amesema kuwa: Wakati Marekani ilipojiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya JCPOA na nchi nyingine zikafuatana nayo, agizo la Qur'ani lilikuwa likisema kuwa nyinyi pia muachane na ahadi zenu, hata hivyo serikali yetu haikuacha kutekeleza majukumu na ahadi zake na ilipunguza utekelezaji wa baadhi ya vipengee vyake ambavyo navyo inaweza kuvitekeleza tena iwapo nchi hizo zitatekeleza majukumu yao.

Kiongozi Muadhamu akihutubia majumbe wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua kiongozi wa juu wa Iran

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Wakati huu muigizaji huyu wa michezo ya kuchekesha na Mzayuni wa kimataifa daima amekuwa akisema kuwa hawatairuhusu Iran kupata silaha za nyuklia, ilhali anapasa kuambiwa kuwa, kama Jamhuri ya Kiislamu ingekuwa na azma ya kutengeneza silaha za nyuklia, yeye na wakubwa zaidi kuliko yeye wasingeweza kuzuia jambo hilo.

Ayatullah Khamenei amesema kitu kinachoizuia Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutengeneza silaha za nyuklia ni fikra na misingi ya Kiislamu ambayo inaharamisha na kuzuia uundaji wa silaha za nyuklia au kemikali zinazosababisha mauaji ya wananchi wa kawaida.   

Amekumbusha mauaji ya umati ya watu laki mbili na elfu 20  yaliyofanywa na Marekani wakati iliposhambulia Japan kwa mabomu ya nyuklia na vilevile mzingiro wa watu wa Yemen na mashambulizi ya ndege za kivita za nchi Magharibi  dhidi masoko, mahospitali na shule za nchi hiyo na kusema: Mauaji ya raia wasio na hatia ndiyo mbinu ya Wamarekani na Wamagharibi, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikubaliani na mbinu hiyo; kwa msingi huo haina nia ya kuunda silaha za nyuklia.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, hata hivyo Iran imeazimia kupata uwezo wa kinyuklia unaoendana na mahitaji ya nchi na kwa sababu hiyo urutubisha madini ya urani hautaishia kwenye kiwango cha asilimia 20, na itachukua hatua wakati wowote itakapohitajika na kwa mujibu wa mahitaji ya nchi, na yumkini ikafikisha urutubishaji huo katika asilimia 60.

Ayatullah Khamenei

Ayatullah Khamenei amesema madai ya silaha za nyuklia ni kisingizio tu, kwa sababu nchi hizo za Magharibi pia hazitaki kuona Iran ikipata hata silaha za kawaida, lakini Wamagharibi wenyewe wanaelewa vyema kwamba, hatuna azma ya kutengeneza silaha za nyuklia. 

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa katika kadhia hii ya nyuklia, kama ilivyo katika kadhia nyingine, Jamhuri ya Kiislamu katu haitalegeza misimamo yake, na itapiga hatua mbele kwa nguvu zote katika njia ya kile chenye maslahi na mahitaji ya leo na kesho ya taifa hili.

Read Entire Article