PERMISSIONS

UN yatafuta dola milioni 266 kuwanusuru wakimbizi milioni tatu katika nchi za Afrika Mashariki

1 month ago 13

Mashirika ya Umoja wa Mataifa yanasaka dola milioni 266 ili kunusuru wakimbizi milioni tatu waliokumbwa na mkato wa mgao kwenye nchi za Afrika Mashariki.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR na lile la Mpango wa Chakula la umoja huo WFP yameeleza hayo kupitia taarifa yao ya pamoja iliyotolewa jijini Nairobi nchini Kenya hapo jana Jumanne.

"Uhaba wa fedha umelazimisha mashirika haya kupunguza huduma zao kwa asilimia 60 na kuna hatari ya wakimbizi kukumbwa na ukosefu wa damu, utapiamlo na udumavu miongoni mwa watoto sambamba na hofu ya ukosefu wa usalama," imesema taarifa hiyo.

Mkurugenzi wa ofisi ya UNHCR kanda ya Afrika Mashariki Clementina Nkweta-Salami anasema janga la Corona limekuwa na madhara makubwa lakini kwa wakimbizi, athari hasi ni maradufu.

Amesema "bila fedha za nyongeza kupatikana, maelfu ya wakimbizi wakiwemo watoto hawatakuwa na chakula cha kutosha. Hofu ya ukosefu wa ulinzi nayo inaongezeka, makato ya mgao wa chakula na fedha yanasababisha wakimbizi washindwe kumudu mahitaji yao ya lazima kama vile chakula, hivyo wanakula mlo mmoja, wanachukua mikopo kwa riba ya juu, wanauza mali zao, watoto wanatumikishwa, vile vile kuongezeka kwa matukio ya ukatili majumbani."

Utoaji msaada wa chakula kwa watoto wakimbizi

Kwa upande wake, Michael Dunford ambaye ni Mwakilishi wa WFP kanda ya Afrika Mashariki anasema ni lazima kuanza kukidhi mahitaji ya chakula na lishe kwa wakimbizi kwenye ukanda huo wa Afrika Mashariki hivi sasa.

Amesema, katu hawajawahi kuwa na kiwango cha chini cha fedha kama wakati huu, "tuna pengo la dola milioni 266 kwa kipindi cha miezi sita kijacho cha kukidhi mahitaij ya wakimbizi. Tuna hofu kubwa kuwa iwapo makato ya mgao yataendelea, wakimbizi watakumbwa na uchaguzi mgumu; kusalia kambini ambako chakula na hali ya usalama havitoshelezi au kurejea nyumbani ambako bado hali ya usalama si nzuri."

Katika nchi 11 zinazohudumiwa na UNHCR kanda ya Afrika Mashariki na pembe ya Afrika na Maziwa Makuu ,asilimia 72 ya wakimbizi milioni 4.2 wanakabiliwa na makato ya mgao wa chakula na misaada mingineyo.../

Read Entire Article