PERMISSIONS

Sisitizo la kusimama kidete Venezuela mbele ya vita vya kiuchumi vya Marekani na Ulaya

1 month ago 21

Kutokana na kuendelea sera za vikwazo za Marekani na madola ya Ulaya, dhidi ya Venezuela, Rais Nicolas Maduro wa nchi hiyo amesisitiza kuwa, nchi yake itaendelea kusimama kidete mkabala wa sera hizo ambazo amesema kuwa ni “vita vya kiuchumi vya pande kadhaa”.

Licha ya uongozi kubadilika nchini Marekani na kuingia madarakani Rais Joe Biden sambamba na udharura wa kuweko ushirikiano wa dunia dhidi ya janga la virus ivy Corona, lakini Washington na washirika wake wangali wanaendeleza vita vya kiuchumi dhidi ya nchi ya Venezuela.

Katika mkondo huo, hivi karibu Baraza la Ulaya liliwaongezea katika orodha yake ya vikwazo maafisa 19 wa ngazi za juu wa serikali ya Venezuela kwa kisingizio kwamba, wamekiuka na kuipaka matope demokrasia.

Kwa hatua hiyo, idadi ya viongozi na maafisa wa ngazi za juu waliopo katika orodha ya vikwazo ya Umoja wa Ulaya sasa imefikia shakhsia 55. Hii ni katika hali ambayo, sehemu muhimu ya uchumi wa Venezuela ikiwemo sekta ya mafuta, petrokemikali na Beki Kuu imewekewa vikwazo na Marekani, huku sehemu kubwa ya mali za nchi hiyo ya Amerika ya Larini ikiwa imezuiwa. Kimsingi ni kuwa, Marekani na waitifaki wake wanafanya kila wawezalo kuubana mduara wa vikwazo na kuishinikiza kiuchumi na kisiasa Venezuela na hivyo kuibua malalamiko ya kijamii nchini humo.

Lengo la yote hayo ni kuandaa mazingira ya kumuondoa madarakani Rais Nicolas Maduro, na hivyo kuhakikisha inaingia madarakani serikali ambayo itafuata malengo ya Marekani katika eneo hilo, hatua ambayo itaiandalia mazingira Washington ya kunufaika na maliasili na vyanzo vya utajiri wa nchi hiyo.

Hili ni jambo ambalo limebainishwa mara chungu nzima na Rais Maduro. Katika msimamo wake wa hivi karibuni kabisa, Rais Nicolas Maduro sambamba na kukosoa kesi 450 za vikwazo za Marekani na Ulaya alisema kuwa, hatua hizo si za kisheria, za usaliti na ni mipango iliyoratibiwa kabla, msimamo ambao umeungwa mkono pia na ripota maalum wa Umoja wa Mataifa.

Alena Douhan, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu, ameashiria katika ripoti yake ya hivi karibuni athari mbaya na zenye madhara za vikwazo vya kiuchumi vya Marekani dhidi ya Venezuela na kusema: Vikwazo dhidi ya sehemu kubwa ya sekta ya viwanda na taasisi za Venezuela vimepelekea kutokea maafa ya kibinadamu na kiuchumi kwa jamii yote ya nchi hiyo ya Latin America hususan tabaka masikini.

Alena Douhan, ripota maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya haki za binadamu,

Licha ya kuwa, ni muda sasa tangu mashinikizo dhidi ya Venezuela yashadidi, lakini kusimama kidete wananchi na himaya na uungaji mkono wao kwa Rais Maduro umepelekea siasa za mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa zifeli na kugonga ukuta. Katika upande mwingine, viongozi wa Caracas wameongeza kasi ya kuwa na ushirikiano na mabadilishano ya kibiashara na waitifaki wake ili kuziba na kufidia pengo linalotokana na vikwazo.

Kuhusiana na hilo, katika miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa kuongezeka pakubwa ushirikiano na mabadilishano ya kibiashara baina ya Jamhuri ya Kiisamu ya Iran na Venezuela. Licha ya vikwazo na vitisho, Iran imeweza kupeleka nchini Venezuela meli kadhaa zilizosheheni mafuta na hivyo kuipiga jeki Venezuela katika suala zima la uhaba wa nishati hiyo muhimu. Aidha Iran imefungua duka kubwa zaidi mjini Caracas la bidhaa na huduma muhimu.

Meli ya mafuta ya Iran ikielekea Venezuela

Kadhalika katika hatua ya hivi karibuni kabisa, ripoti zinasema kuwa, kupitia mkataba wa mafuta baina ya Iran na Venezuela, imeafikiwa kuwa, taifa hilo la Amerika ya Latini litaipatia Iran mafuta ya ndege mkabala na nishati ya mafuta ya taifa hili inayosafirishwa kuelekea katika nchi hiyo.

Ala kuli haal, licha ya kuwa viongozi wa Marekani na waitifaki wao wa Ulaya wana matumaini kwamba, vikwazo dhidi ya nchi kama Venezuela vitalifanya taifa hili lisalimu amri na kufuata siasa na matakwa ya mataifa hayo, lakini inaonekana hizo ni ndoto za alinacha; kwani viongozi wa Caracas wanafanya juhudi za kutekeleza sera na mikakati mbalimbali ili kuhakikisha kuwa, wanafidia nakisi na kupunguza makali ya mashinikizo dhidi ya raia wa nchi hiyo yanayotokana na vikwazo vya Marekani na washirika wake wa Ulaya.

Read Entire Article