PERMISSIONS

Mfahamu msichana aliyeanza kutumia mihadarati akiwa na miaka 12

1 week ago 23

Dakika 6 zilizopita

Latifa Said

Chanzo cha picha, Latifa Said

Maelezo ya picha,

Latifa Said alianza kutumia mihadarati akiwa na miaka 12

Maisha ya Everlyne Watere maarufu Latifa Said kutoka mwambao wa Pwani nchini Kenya, yanaweza kuigizwa kwenye tamthilia au filamu. Je ni kwanini iwe hivyo?

Latifa Said alianza kutumia mihadarati akiwa na umri wa miaka 12 katika darasa la 6. Bila shaka alikuwa ni binti mdogo sana, lakini ukweli ni kwamba huo ndio uliokuwa mwanzo wa safari yake ya kuwa mtumiaji wa dawa za kulevya hauwezi kufutika, asijue kwamba, vile vile ulikuwa utangulizi wa mengi maishani mwake ikiwemo kuhatarisha maisha yake.

“Maisha yangu yote nimelelewa Ukunda, kaunti ya Kwale. Nikiwa darasa la tano, ndipo mambo yalianza kubadilika. Nilikuwa sipendi kutangamana na mabinti wenzangu, kwa hio rafiki zangu wengi walikuwa wavulana. Miongoni mwa tuliyokuwa tunajihusha nayo ni kwenda baharini kujivinjari kwa kucheza soka,” Latifa anakumbuka.

Mwanadada huyo anasema kwamba mmoja kati ya rafiki zake wa kiume, kwao nyumbani kulikuwa na watu ambao ni walanguzi wa dawa za kulevya.

Anakumbuka wakitumika kusafirisha dawa hizo kila Jumapili kutoka upande wa Kwale hadi Mombasa nchini Kenya.

Latifa anasema kuwa wakati wakitekeleza shughuli hiyo ya kusafirisha dawa za kulevya, walijipata wameshikwa na tamaa ya kuonja walichokuwa wanabeba na huo ndio ulikuwa mwanzo wa kuharibikiwa na maisha.

“Mara yangu ya kwanza kuonja ‘unga’ ni wakati nimeingia darasa la sita, tulianza kwa kunusa tukiwa katika fukwe za Bahari Hindi upande wa Ukunda. Na pia katika shule hiyo ya msingi, nilikuwa natembea na kundi la wavulana 5 ambao tulitumia dawa hizo darasani au tukiwa kwenye vyoo vya wavulana,” anakumbuka Latifa.

Cha ajabu mwanadada huyo anasema, hakujali kuhusu tabia ya kuingia vyoo vya wavulana ila ilifika wakati walimu wakagundua tabia hio na kumshurutisha kueleza sababu. Ilibidi awe mcheshi na kutumia hila ili kuficha siri ya utumiaji dawa za kulevya.

Chanzo cha picha, Latifa Said

Maelezo ya picha,

Latifa Said alifanya ukahaba kukidhi mahitaji yake ya matumizi ya dawa za kulevya.

Kutumbukia mzima mzima katika utumiaji wa mihadarati

Baada ya kisa hicho, Latifa alijikuta ameingilia ulimwengu wa utumiaji mihadarati na hapo ndipo alianza kuwa mraibu. Kufumba na kufumbua akawa amenaswa kwenye mtego huo bila kujua namna ya kujinasua. Haikuchukua muda kwa uraibu huo kuanza kulemaza masomo yake.

“Siku moja baada ya kurudi nyumbani nikiwa kidato cha pili, nikaamua kumueleza mama yangu kwamba hapo nilipofikia ndio utakuwa mwisho wa safari yangu ya masomo. Na kama alikuwa na haja sana ya mimi kusoma, basi, yuko huru kuendelea kutoka nilipoachia. Mama alinishangaa sana, akokasa cha kunijibu kwa maneno makali niliyomtolea. Na kuanzia hapo ikawa ni mvutano kati yangu na wazazi, kwanza kwasababu nilikuwa simuogopi yeyote, na pili, lengo langu lilibadilika na kuamua kuanza maisha ya kutegemea mihadarati siku moja baada ya nyingine,” anasema Latifa.

Ili kukidhi mahitaji yake ya kutumia dawa za kulevya alianza hila mbalimbali kwa mfano, kudanganya wazazi kuhusu matukio fulani kwa nia ya kupate pesa za kununua mihadarati.

Na kwa kuwa tayari alikuwa amesusia masomo, alitumia njia za mkato zaidi kama wizi mdogo mdogo na pia utapeli wa kimapenzi.

“Hawa wanaume nilikuwa nawaibia mno. Kitu cha kuchukiza zaidi ni kuwa dawa hizi za kulevya zitakupa ujasiri na kuwaibia waziwazi tu. Sasa hivi kuna wakati huwa nakaa chini na kuanza kujiuliza, nilifaulu vipi kufanya vitendo vile bila kujali ubinadamu? ila ukiwa unatumia ‘unga’ utajipata hujali Kabisa,” anasema Latifa.

Alikuwa na tabia ya kunyemelea ndani ya nyumba za watu wakati wako kwenye shughuli zao au ikiwa wamesahau kufungo milango yao. Anaingia na kupora chochote atakachokutana nacho lengo likiwa ni kukiuza ili apate pesa za kununua dawa za kulevya.

Aidha, mwanadada huyo anakiri kwamba ukahaba alioufanya ulikuwa tu wa kukidhi mahitaji yake ya matumizi ya dawa za kulevya.

Chanzo cha picha, Latifa Said

Maelezo ya picha,

Licha ya kwamba Latifa Said ameamua kubadilisha maisha yake ana hofu ya kurejelea tena dawa hizo.

Latifa anapohesabu miaka aliyoipoteza katika ulimwengu huo kwa kutekwa na dawa za kulevya hujutia sana, kwasababu kwa hesabu zake za haraka haraka, miaka 24 ya maisha yake anaihesabu kama iliyopotea bure, bila kufanya lolote la msingi maishani.

Latifa anasema sio maisha anayomtakia hata adui yake. Kingine ni kuwa hakuna siku hata moja aliyoweza kutekeleza shughuli zake bila kutumia dawa za kulevya, kwa mfano, kupata usingizi ilikuwa ni kibarua kigumu kwasababu ilifika wakati ikawa, ili apate angalau lepe la usingizi ni lazima awe amepata dozi yake.

Hata hivyo, licha ya yote aliyopitia, Latifa ana kile anachojivunia.

“Nashukuru kuwa miaka hiyo 24 imepotea bila kuafikia malengo ya kawaida ya kibinadamu, lakini nilijaaliwa kupata wanangu wanne. Wajua sio wanawake wengi wanaokuwa waraibu wa mihadarati hupata watoto, kisa na maana wanakosa muda. Kuna wenzangu wengi wanawake waliokuwa waraibu ambao walifariki dunia bila kuzaa,” Latifa anasema.

Kingine ambacho huenda hukifahamu ni kwamba mwanamke huyo anakiri alipokuwa anaanza kutumia ‘unga’ aliuhisi ukiwa mtamu sana, ila baada ya kuwa mtegemezi wa dawa hizo, alianza kuhisi ukiwa mchungu kweli. Anajutia maisha ya nyuma na amejitolea kuwa funzo sio tu kwa jamii lakini hata kwa watoto wake pia.

“Kwa miaka kumi ya maisha yangu nilitoroka nyumbani na kuishi kama asiye na kwao. Nilikuwa naona haya hata kufika kwetu, nilitamani niwaone watoto wangu lakini nilikaa mbali na wao kwa aibu niliyokuwa nayo. Sikutamani kukaa na watu wa kawaida kwa kuogopa wanasema nini kunihusu?,”anakumbuka Latifa.

Mui huwa mwema

Chanzo cha picha, Latifa Said

Maelezo ya picha,

Watoto wake ndio waliomshawishi Latifa Said kuanza kubadilika

Miaka miwili na nusu iliyopita, Latifa alikubali kushirikiana na shirika moja kwa jina ‘Reach Out’ lililopo mjini Mombasa kuanza mchakato wa kujinasua kuachana na uraibu wa dawa za kulevya.

Latifa anasema sio jambo rahisi na changamoto kuu kwake ni mwili kupigana na dawa hizo alizokuwa akizitumia.

Latifa anakiri kuwa watoto wake ndio waliompa ujasiri wa kuchukua hatua za kuacha kutumia dawa hizo.

“Niliwaza kuwa sasa, hawa wanawangu wamenifahamu kama mama mlevi na mwenye vituko vya kila aina, je inawezekana nikawapa taswira nyingine kunihusu? Nilijiambia, na kuanzia hapo nimepigana mno kubadilisha maisha yangu nionekane kama mama anayetekeleza majukumu yake na pia kudhihirishia umma kwamba mui anaweza kuwa mwema.

Latifa anaongeza kuwa kuingia kwenye uraibu wa dawa za kulevya au uraibu mwingine wowote ule, ni rahisi na huonekana kuwa jambo jepesi, ila mtu anapotekwa huwa ameingia kwenye mtego ambao ni mgumu kutoka.

Pia changamoto nyingine inayomkabili Latifa, ni kukubalika tena katika jamii na kupata ajira licha ya kwamba ameamua kubadilisha maisha yake na hata hofu ya kurejelea tena dawa hizo.

Latifa anatoa ushauri nasaha kwa wazazi wenye watoto kuwa makini na kufuatilia mienendo yao kwani huchukua muda mrefu kwa wazazi kugundua kuwa watoto wao wanatumia dawa za kulevya wakati tayari maji huwa yameshamwagika.

Read Entire Article