PERMISSIONS

Marekani yashambulia maeneo ya wapiganaji Syria

1 month ago 22

Wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon  imesema kuwa Rais Joe Biden ndiyo ameamuru kufanyika mashambulizi hayo ya anga katika eneo la udhibiti wa mpakani linalotumiwa na makundi ya wanamgambo yanayofadhiliwa na Iran mashariki mwa Syria kama vile Kait’ib Hezbollah na Kait’ib Sayyid al-Shuhada. Hiyo ni hatua ya kwanza ya kijeshi kuchukuliwa na Rais Biden tangu alipoingia madarakani dhidi ya miundombinu ya wapiganaji hao.

Waliohusika na mashambulizi wapongezwa

Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin amesema wana uhakika kuhusu mashambulizi hayo kwamba yamefanyika kwenye maeneo yanayotumiwa na waasi.

”Niseme tu kwamba ninajivunia wanajeshi wetu waliotekeleza shambulizi. Kama mnavyotarajia wamefanya kwa kuzingatia utaalamu sana na tunashukuru kwa huduma yao. Tunajua kwamba maeneo tuliyoyalenga yalikuwa yanatumiwa na kundi hilo hilo la wanamgambo wa Kishia ambalo limefanya mashambulizi dhidi ya Wamarekani walioko Iraq,” alifafanua Austin.

Maafisa wa Marekani awali hawakufafanua kama kulikuwa na wahanga wowote kutokana na mashambulizi hayo nchini Syria. Hata hivyo shirika la kufatilia haki za binaadamu nchini Syria limesema kuwa wapiganaji 22 wa Iraq wanaoungwa mkono na Iran wameuawa katika mashambulizi hayo.

USA I Joe Biden unterzeichnet Executive Order

Rais Joe Biden (aliyeketi) na Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Lloyd Austin

Pentagon imesema kuwa Marekani ilishauriana na washirika wake walioko kwenye vikosi vya muungano kabla ya kuchukua hatua hiyo na operesheni hiyo ilipeleka ujumbe kwamba Biden atachukua hatua kuwalinda Wamarekani na washirika wake wa muungano. Wizara hiyo ya ulinzi ya Marekani imesema mashambulizi hayo yamefanyika kujibu mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa dhidi ya wanajeshi wa Marekani na maeneo ya kibalozi nchini Iraq.

Mashambulizi ya nyuma

Katikati ya mwezi Februari, roketi kadhaa ziirushwa katika kambi ya jeshi la Marekani iliyoko kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Irbil kwenye jimbo linaloendeshwa na Wakurdi kaskazini mwa Iraq. Shambulizi hilo lilimuua mkandarasi mmoja raia wa kigeni na kuwajeruhi wafanyakazi wa Marekani pamoja na wanajeshi wengine walioko kwenye jeshi la muungano.

Siku ya Jumatatu shambulizi jengine la roketi lilililenga eneo lenye ulinzi mkali maarufu kama Green Zone kwenye mji mkuu wa Iraq, Baghdad, ambako kuna ofisi za serikali na balozi za mataifa ya kigeni, ikiwemo Marekani. Hata hivyo, ingawa kundi la Kait’ib Hezbollah halikukiri kuhusika na mashambulizi hayo ya roketi, Waziri Austin amesema nchi yake inaamini kwamba kundi hilo linahusika.

Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Javad Zarif amezungumza kwa njia ya simu na waziri mwenzake wa Syria, Faisal al-Miqdad saa chache baada ya mashambulizi hayo ya Marekani. Pande hizo mbili zimesisitiza umuhimu wa mataifa ya Magharibi kuyazingatia maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Syria.

(DPA, AP, AFP, Reuters)

Read Entire Article