PERMISSIONS

Kushadidi chuki dhidi ya Uislamu na kuenea vitendo vya utumiaji mabavu katika ulimwengu wa Magharibi

1 week ago 22

Kuenea chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia) katika ulimwengu wa Magharibi hivi sasa limegeuka na kuwa tatizo kubwa na la kijamii, tatizo ambalo limeibua na kushadidisha vitendo vya utumiaji mabavu katika jamii ya Magharibi.

Kuhusiana na hilo,  Jeremy Corbyn, mwanasiasa wa Uingereza na kiongozi wa zamani wa chama wa Leba amekiri kwamba, chuki dhidi ya Uislamu katika ulimwengu wa Magharibi zimeshika kasi na kuchukua wigo mpana na kwamba, Waislamu wamekuwa wakiandamwa na vitendo hivyo. Mwanasiasa huyo anasisitiza kwamba, kuna ulazima wa kukabiliana na kasi ya kuenea vitendo vya chuki dhidi ya Uislamu na hatua mbalimbali za uenezaji uhasama na uadui katika ulimwengu wa Magharibi.

Vitendo vichafu vya kampeni za chuki dhidi ya Uislamu vimeongezeka mno katika miaka ya hivi karibuni huko nchini Marekani na barani Ulaya. Katika miaka ya hivi karibuni viongozi wa Ulaya walifanya kila wawezalo kuwafungamanisha na ugaidi Waislamu wanaoishi barani humom na hivyo kuhalalisha mapungufu ya kiusalama na kisiasa yanayoisumbua jamii ya Magharibi. Katika uga huu tunaweza  kuashiria matukio kama ya kuvunjiwa heshima Mtume (saw), Qur’ani Tukufu, kuwapachika jina la ugaidi Waislamu, kuamiliana vibaya na wafuasi wa dini ya Uislamu, utumiajui mabavu na ubaguzi wa polisi dhidi ya Waislamu na kupasishwa sheria  ambazo kimsingi zinalenga kuwabana na kuwakandamiza Waislamu.

Mashinikizo haya yamewafanya hata baadhi ya viongozi wa Ulaya wajitokeza na kuelezea wasiwasi walionao kuhusiana na mashinikizo dhidi ya Waislamu na kulitaja hilo kama chimbuko la kukua harakati za wafuasi wa mrengo wa kulia na wenye misimamo ya kuchupa mipaka, na vilevile kuongezeka vitendo vya utumiaji mabavu katika mataifa hayo.

Maandamano ya kupinga chuki dhidi ya Uislamu

Kwa mujibu wa ripoti ya kundi la Waislamu katika Bunge la Uingereza ni kuwa, kuenea chuki dhidi ya Uislamu katika nchi hiyo ya bara Ulaya kumepelekea kushadidi tofauti za kimatabaka katika jamii na kukithiri uhalifu unaohusiana na chuki na mashambulio ya kigaidi. Sehemu moja ya ripoti hiyo inabainisha kwamba: Fikra za waliowengi nchini Uingereza zimekuwa na mtazamo wa kiubaguzi kuhusiana na itikadi za Waislamu na hilo limetokana na utoaji hukumu wa kabla hata ya kufanya kosa unaofanywa dhidi ya wafuasi wa dini hii tukufu.

Gazeti la The Guardian la Uingereza hivi karibuni lilitahadharisha kwamba, chuki dhidi ya Uislamu (Isamophobia) zimeongezeka nchini Uingereza na kumekuwa kukifanyika mibinyo ya kuratibiwa dhidi ya Waislamu.

Hali hii imevifanya vyama vya mrengo wa kushoto na wanasiasa wa polisi katika nchi za Ulaya  kama Ujerumani na Ufaransa kutumia vibaya hali hii na kwa kuzingatia kukaribia chaguzi katika mataifa hayo, wanalitumia hilo kama karata ya kupata kura na hivyo kufungua vinywa vyao na kuwataja Waislamu kama chanzo cha ugaidi, tatizo la ajira na ukosefu wa usalama na amani katika nchi hizo.

Katika uwanja huo, nchini Ufaransa Rais Emmanuel Macron wa nchi hiyo akiwa na lengo la kuwaridhisha wapiga kura wamchague katika uchaguzi ujao miezi michache ijayo sambamba na kutumia msamiati wa "Ugaidi wa Kiislamu" ametangaza kuunga mkono kikamilifu sheria zinazowabana Waislamu. Nchini Ujerumani pia hivi karibuni kulipasishwa sheria ambayo inapiga marufuku mabinti wa Kiislamu kuvaa vazi tukufu la hijabu wakiwa katika idara za serikali na vituo vya polisi.

Maandamano ya kupinga matamshi ya chuuki dhidi ya Uislamu ya Rais wa Ufaransa 

Hii ni katika hali ambayo, katika miezi ya hivi karibuni kutokana na masaibu ya janga la Covid-19, mabadiliko ya kisiasa na kushadidi matatizo ya kiuchumi ulimwenguni kote, vitendo vya utumiaji mabavu katika jamii ya Magharibi vimeshadidi mno. Picha zilizosambazwa hivi karibuni nchini Ufaransa zikionyesha wananchi wakiandamana kulalamikia sheria kali za kukabiliana na janga la Corona ni mfano wa wazi kuhusiana na jambo hili.

Filihali Ulaya na ulimwengu wa Magharibi kwa ujumla yanakabiliwa na tatizo kubwa katika uga wa usalama na siasa. Malalamiko ya kijamii yameongezeka mno katika mataifa hayo na bila shaka madai yao ya uhuru wa kutoa maoni, utendaji wa chuki dhidi ya Uislamu na kanuni kali za kuwabinya Waislamu wanaoishi katika nchi hizo ni mambo ambayo hayakubaliwi tena na fikra za waliowengi katika nchi hizo. Hiyo ni hatari ambayo sasa baadhi ya viongozi na wanasiasa wa Ulaya wameidiriki na kutoa indhari kuhusiana nayo.

Tony Blair Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza amekiri bayana kwamba, dini ya Uislamu haina mfungamano na ugaidi, chuki na misimamo ya kuchupa mipaka na amewahimiza Waislamu kukabiliana na chuki na misimamo mikali.

Ukwekli wa mambo ni kuwa, hivi sasa siyo Waislamu tu wanaoishi katika mataifa ya Magharibi ndio wanaokabiliwa na vitendo vya chuki  dhidi ya Uislamu na utumiaji mabavu, bali hali hii ya chuki, hasama na utumiaji mabavu imeongezeka na kutanda pia katika anga ya kijamii ya mataifa hayo; jambo ambalo limewafanya baadhi ya viongozi wa Ulaya kama Jeremy Corbyn ajitokeze la kutahadharisha kuhusiana na jambo hilo.

Read Entire Article