PERMISSIONS

Jumanne tarehe 14 Septemba 2021

1 week ago 14

Leo ni Jumanne tarehe 7 Safar 1443 Hijria inayosadifiana na tarehe 14 Septemba 2021.

Katika siku kama ya leo miaka 1393 iliyopita, yaani tarehe 7 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw). Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo wa umri wake pamoja na babu yake, Mtume Muhammad (saw) ambapo alinufaika na mafunzo na maarifa ya dini tukufu ya Kiislamu. Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as). Baada ya kuuliwa Imam Ali (as), Waislamu walimpa baia na mkono wa utiifu Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza;  hata hivyo baada tu ya kushika hatamu alikabiliwa na njama na uasi wa Muawiyah bin Abi Sufiyan. Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi kwa ajili ya kukabilina na uasi wa Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah. Imam Hassan al Mujtaba (as) alilazimika kufanya suluhu na Muawiyah bin Abi Sufiyan kwa ajili ya kulinda maslahi ya Uislamu na Waislamu. Mjukuu huyo kipenzi wa Mtume (saw) aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufiyan.

Siku kama ya leo miaka 209 iliyopita, moja kati ya matukio makubwa ya moto uliowashwa kwa makusudi ulimwenguni lilitokea katika mji mkuu wa Russia, Moscow. Tukio hilo lilitokea baada ya kupita siku moja tu, tangu mji huo uvamiwe na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte, wakati mji huo ulipochomwa moto kwa amri ya mtawala wa wakati huo wa mji huo. Lengo la mtawala huyo lilikuwa ni kuyafanya majeshi ya Bonaparte yashindwe kustafidi na suhula za mji huo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji mzima wa Moscow. 

Moto mkubwa wa Moscow

Miaka 61 iliyopita katika siku kama ya leo, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudi Arabia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo.

Katika siku kama ya leo miaka 43 iliyopita yaani tarehe 23 Shahrivar mwaka 1357 Hijria Shamsia kulifanyika maandamano makubwa hapa nchini kuwaenzi mashahidi waliokuwa wameuawa na vibaraka wa Shah siku kadhaa kabla yake. Siku hiyo umati mkubwa wa watu ulimiminika katika makaburi ya Behesht Zahraa mjini Tehran kuwaenzi mashahidi hao. Askari wa utawala wa Shah walikuwa na nia ya kuzuia maandamano hayo lakini umati mkubwa wa wananchi walioshiriki maandamano ulidumisha malalamiko yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah huko wakipiga nara za: “Iran ni nchi yetu na Khomeini ni kiongozi wetu.” 

Siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 7 Safar 1411 Hijria alifariki dunia Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi mmoja wa Marajii na viongozi wa juu wa Kiislamu hapa nchini, akiwa na umri wa miaka 96. Alimu huyo alisoma elimu za fiqihi, usul fiqihi, hadithi, tafsiri ya Qur'ani, teolojia na misingi ya kimaadili katika vyuo vikuu vya kidini katika miji ya Kadhimain na Najaf nchini Iraq. Miongoni mwa athari kubwa zilizoachwa na Ayatullah Mar-ashi Najafi ni maktaba kubwa ya vitabu iliyoko katika mji wa Qum, ambayo inahesabiwa kuwa ya aina yake na ina vitabu zaidi laki tatu. 

Ayatullahil Udhma Sayyid Shahabuddin Mar-ashi Najafi
Read Entire Article